EXCLUSIVE VIDEO: SHAFFIH AMTAJA KOCHA ANAYEFAA LIVERPOOL
Baada ya kupigwa kwa pambano la Merseyside derby mwishoni mwa juma lililopita kati ya Everton dhidi ya Liverpool na kumalizika kwa sare ya timu hizo kufungana goli 1-1 kwenye dimba la Goodson Park, aliyekuwa kocha mkuu wa Liverpool ‘majogoo wa jiji’ Brendan Rodgers alifungashiwa virago.
Lakini kitu kikubwa baada ya hapo ilikuwa ni nani atarithi mikoba iliyoachwa na kocha huyo huku watu wengi wakionekana kumpigia upatu kocha wa zamani wa Borussia Dortmund Jurgen Klopp pamoja na muitaliano Carlo Ancelotti.
“Mimi kwa mtazamo wangu, hawa makocha wote wawili wana historia nzuri sana siku za nyuma wakiwa wamefundisha vilabu kadhaa. Lakini mimi kama napewa nafasi ya kufanya uchambuzi wa kuamua ni kocha yupi ambaye anahitajika Liverpool katika kipindi hiki, bila shaka kura yangu ingeangukia kwa Carlo Ancelotti”.
“Kwasababu mbali na kwamba Ancelotti ni moja kati ya makocha ambao wamepata mafanikio makubwa, lakini tayari anauzoefu wa kutosha ukilinganisha na Klopp. Lakini ukiachana na hilo, Ancelotti amefundisha pia kwenye ligi ya England mwaka 2009-2010 akiwa na Chelsea na kuiongoza kuchukua taji la EPL”.
“Liverpool ina historia ya kunyakua mataji matano ya UEFA Champions League (kombe la vilabu bingwa barani Ulaya), kocha huyu ana historia ya kuchukua taji hilo akiwa na AC Milan pamoja na Real Madrid. Lakini pia kwenye mataji ya ligi ya nchi husika (domestic tittles) amefanya vizuri”.
“Amekwenda nchini Ufaransa kuifundisha PSG timu yenye mstaa wengi akaangalia mahitaji ya wawekezaji kwenye timu hiyo walikuwa wanataka nini katika kipindi hicho, katika mwaka mmoja aliokaa kwenye klabu hiyo akafanikiwa kutwaa ubingwa wa nchi hiyo japo kwenye Champions League hakufanya vizuri sana”.
“Kuchukua ubingwa wa Champions League inahitaji muda wa kukaa na timu ili kutengeneza muunganiko mzuri ‘chemistry’ ya wachezaji ambayo inaweza kufanya timu iwe ya ushindani na kupambana na vilabu kama Bayern Munich, FC Barcelona, Real Madrid na vinginevyo”.
Kwa kifupi mimi nampa nafasi Carlo Ancelotti kwasababu ya uzoefu aliokuwanao lakini pia style yake ya ufundishaji. Ni mtu ambaye hana haraka, msikivu, utendaji wake unarahisisha wachezaji kuchukua mbinu kirahisi na kutekeleza uwanjani.
“Kwa upande wa Jurgen Klopp, yeye ni kijana kwasasa ana umri wa miaka 48 amepata mafanikio makubwa sana akiwa na Borussia Dortimund na ndio timu ambayo imempa jina. Amechukua ubingwa wa Bundesliga mara mbili wakati ambao Bayern Munich walikuwa hawako katika wakati mzuri”.
“Huwezi kumlaumu moja kwa moja kwa Dortmund kufanya vibaya miaka michache baadae kutokana na wachezaji wenye majina makubwa kuchukuliwa na Bayern Munich na kwenda kuimarisha zaidi upande wa pili”.
“Watu wengi pia wamekuwa wakimpigia ‘debe’ apewe timu ya Liverpool, nadhani kocha huyu anaweza akafanya vizuri zaidi akiwa Ujerumani kuliko England kwani kuna namna ya kucheza na vvombo vya habari, namna ya kuwapa Liverpool wanachotaka kwa sasa. Kwasababu wote tunajua ni miaka 25 imepita sasa bila kutwaa taji la EPL na hicho ndio kipaumbele chao kwa sasa”.
“Kwahiyo Klopp akija pale atabebeshwa mzigo mkubwa, kumbuka hajawahi kupata presha kubwa kwani wakati yupo na Dortmund alipata mafanikio makubwa huku akiwa hana presha kubwa kutokana na kupata muda wa kutosha kuiandaa timu na walimruhusu kufanya hivyo na kufanikiwa kufanya vizuri”.
“Lakini inapokuja Liverpool, hawana muda wa kusubiri wanataka matokeo. Na mtu wa kuja kufanya mapinduzi ya muda mfupi na muda mrefu ni Carlo Ancelotti kocha wa kimataifa kutoka Italia”.
No comments